Swahili articles

RUTO ANAVYOMDHIBITI RIGATHI KWA BUSARA

todayJune 20, 2023 85 1

Background
share close

Siku zote ati palipo na wazee hapaharibiki jambo, wahenguzi hawakuambulia patupu.

RAIS William Ruto hajakuwa mwepesi kumruhusu Naibu wake Rigathi Gachagua kuongoza uzinduzi wa miradi mikubwa ya miundomsingi tangu alipoingia mamlakani Septemba 13, 2022 hali ambayo imeibua maswali mengi sana miongoni mwa wakenya.

Sababu ni kwamba hali hii ni tofauti kabisa muhula wa kwanza wa utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta. Nyakati hizo, Dkt Ruto akiwa Naibu Rais, sawa na Gachagua, alipewa uhuru wa kuzunguka kote nchini akizindua miradi ya maendeleo, hususan, barabara.

Ni kutokana uhuru huo wa kuzuru maeneo kadha nchini akazindua miradi ya maendeleo ambapo Bw Kenyatta alibuni neno “Tangatanga” kurejelea mtindo wa Dkt Ruto wa kuzuru sehemu mbalimbali nchini akizindua miradi ya serikali, na kuongoza mikutano ya harambee haswa makanisani.

“Mkimuona huyu naibu wangu akipitia hapa anapotangatanga hapa na pale muelezee shida zenu,” Rais Kenyatta akasema mnamo Aprili 7, 2018 kwenye mkutano wa hadhara katika eneo bunge la Embakasi Mashariki, kaunti ya Nairobi.

Wakosoaji wa Dkt Ruto walidai tangu mwaka wa 2013 walipoingia afisa na Bw Kenyatta, kiongozi huyo alikuwa akitumia hafla hizo za uzinduzi wa miradi ya serikali kama majukwaa ya kujinadi kisiasa kwa kufanikisha ndoto yake ya urais.

Hatimaye mnamo Septemba 23, 2018 Bw Kenyatta alishawishika kuwa ni kwamba Dkt Ruto, kama naibu wake alikuwa akitumia uzinduzi wa miradi ya serikali kama vile barabara kama kisingizio za kujikuza kisiasa.

Hii haswa ni baada ya Dkt Ruto kuonekana kukerwa na handisheki kati yake na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, mapema mwaka huo.

Ndiposa mnamo Januari 19, 2019 Bw Kenyatta alifanya mabadiliko katika serikali yake na kumteua aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri kuhusu Utekelezaji wa Miradi ya Serikali Kuu.

Aidha, Rais Kenyatta, wakati huo, aliamuru hamna afisa wa serikali ataruhusiwa kuzindua miradi ya serikali kote nchini bila idhini ya kamati hii na makamishna wa kaunti. Lakini hatua hii ilionekana kumlenga naibu wake wakati huo, Dkt Ruto.

Sasa wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema ni kutokana na tajriba ya Rais Ruto chini ya urais wa Bw Kenyatta ambapo ameamua kumnyima Bw Gachagua nafasi ya kuzindua miradi ya serikali asije akatumia nafasi hiyo kujinadi kisiasa na hivyo kupovuruga “hesabu zake za kisiasa” kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

“Rais Ruto hataki kurejelea ‘makosa’ ambayo mtangulizi wake hali iliyompa yeye kama naibu Rais wakati huu kujitia makali kisiasa. Bw Gachagua amejitokeza wazi kuonyesha nia ya kumrithi Uhuru kama kinara wa kisiasa eneo la Mlima Kenya. Ndoto hii ni hatari kwa Rais Ruto ambaye anataka kuendelea kuwa na usemi wa kisiasa eneo hili lenye utajiri mkubwa wa kura,” anasema Bw Martin Andati.

“Hii ndio maana tangu alipoingia mamlakani mwaka 2022, Dkt Ruto amehakikisha kuwa yeye ndiye anazindua miradi mikubwa ya serikali hata katika eneo la Mlima Kenya wala sio Bw Gachagua,” anaongeza mchanganuzi huyo wa masuala ya kisiasa na uongozi.

Kwa mfano tangu Kenya Kwanza kuingia mamlakani, ni Rais Ruto mwenyewe ndiye amekuwa akiongoza hafla za uzinduzi wa miradi ya miundo msingi kama vile barabara na mabwawa.

Mnamo Aprili 7, mwaka huu Rais Ruto alizuru kaunti ya Nyandarua ambapo alizindua mradi wa kuwekwa lami kwa barabara ya Captain-Ndemi/Wanjohi-Kwa Matu-Geta-Kahuruko-Ndunyu Njeru yenye umbali wa kilomita 55.

Rais aliandamana na naibu wake Bw Gachagua, pamoja na viongozi wa eneo hilo.

SIKU ZOTE MJA HUJITWALIA BUSARA KUTOKANA NA WAJIBU WAKE.



Written by: 254 Radio

Rate it

Previous post

News

MAKALI NDANI YA MSAWADA WA FEDHA MWAKA WA 2023 NA MAJIMBO KIBAYASI

WAMILIKI wa biashara ndogo kama vile mama mboga na wahudumu wa bodaboda ni miongoni mwa Wakenya watakaofinywa na makali ya ushuru uliopendekezwa na bajeti ya kwanza ya Rais William Ruto. Iwapo Mswada wa Fedha wa 2023 utapitishwa na Bunge, wamiliki wa biashara ndogo ambao wamekuwa wakiuza bidhaa za angalau Sh1,400 kwa siku watalazimika kulipa asilimia tatu ya mauzo hayo. Ikiwa mfanyabiashara anatoa huduma au bidhaa za Sh1,400 kila siku inamaanisha […]

todayJune 3, 2023 109 1

0%